Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TAMBUA SOKO, ONGEZA TIJA, TEKELEZA DIRA 2050

  • August 8, 2026

Dodoma | 8 Agosti, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa Mgeni Rasmi katika Sherehe za Kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nane Nane 2026, yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, Dodoma.

Akihutubia katika kilele hicho, Mhe. Rais alisisitiza umuhimu wa sekta ya kilimo kuendelea kujielekeza katika uzalishaji wenye tija unaoongozwa na mahitaji ya soko, sambamba na kuongeza thamani ya mazao ili wakulima na wazalishaji wanufaike zaidi na fursa za biashara za ndani na nje ya nchi.

Msisitizo huo unaendana na kaulimbiu ya Maonesho ya Nane Nane 2026: “Tambua Soko; Ongeza Tija, Tekeleza Dira 2050” – ikihamasisha matumizi ya teknolojia, ubunifu, na kuimarisha mnyororo wa thamani ili kilimo kiwe biashara yenye tija na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bw. Ephraim Balozi Mafuru, alieleza kuwa TanTrade imejidhatiti kutekeleza dhima ya kaulimbiu hiyo kupitia ushiriki wake katika Nane Nane. Alibainisha kuwa TanTrade itaendelea kuhamasisha uzalishaji unaozingatia soko, uongezaji thamani, ufungashaji bora, na kuwaunganisha wazalishaji na masoko ya ndani na kimataifa. Kupitia kampeni ya Made in Tanzania, TanTrade inalenga kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aidha, Mafuru alisisitiza kuwa TanTrade itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo na viwanda ili kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuvutia uwekezaji, na kuendeleza teknolojia za uchakataji wa mazao na bidhaa za mifugo. Hatua hizi zinalenga kuongeza kipato cha wakulima, kupunguza upotevu wa mazao, na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya kikanda na ya kimataifa.