Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania

TanTrade Fostering Business

TANTRADE TAASISI MUHIMU KATIKA KUCHOCHEA UKUAJI WA SEKTA YA BIASHARA NA UCHUMI NCHINI

  • December 21, 2025

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Patrobas Katambi ameipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwaahidi ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza leo Desemba 20, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akiongea na Menejimenti ya TanTrade, amesema kuwa, uwepo wa  TanTrade ni muhimu  kwa Wizara ya Viwanda na Biashara  kwani inachochea ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara inayosaidia kupata  wawekezaji wengi kwenye maeneo ya Viwanda ,na katika kukuza Biashara za wajasiriamali wadogo, wa kati na hata wakubwa.
Mhe. Katambi amesisitiza, umuhimu wa jukumu la TanTrade katika kushauri Serikali, hivyo ni wajibu wa Mamlaka kutekeleza majukumu kwa weledi uaminifu na umakini mkubwa ili kusaidia uchumi wa nchi kwa kuongeza pato la Taifa, ajira na fursa za mitaji kwa wafanyabiashara wetu. Vilevile, ili kupata taarifa halisi na thabiti, Taasisi iwekeze katika kufanya tafiti na kuratibu masuala ya biashara ndani na nje ya nchi ili kuhakiksha bidhaa za Tanzania zinapata masoko ya uhakika. 

Awali akimkaribisha Naibu Waziri huyo, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa M. Khamis amesema TanTrade ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wadau wa biashara na itaendelea kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara  katika kufanikisha maono ya Serikali, kuhakikisha biashara zinaimarika na bidhaa kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.